Tuesday, 4 March 2014

Mauzo ya IPTL yamwibua Zitto

Mauzo ya IPTL yamwibua Zitto
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, ameeleza kushtushwa na taarifa za mauzo ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa Kampuni ya Pan Africa Power Limited.
Katika taarifa yake kwa mtandao wake wa kijamii, Zitto, aligusia matumizi ya fedha za akiba maalumu (escrow account) iliyokuwa Benki Kuu (BoT) na hivyo kwa nafasi yake ameomba Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi.
Zitto alisema kwa mujibu wa mkataba kati ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco) na IPTL, gharama ya kukodi mitambo (capacity charge) inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na mkopo wa asilimia 22.31.
“Mtaji wa IPTL ulikuwa dola za Marekani 50 tu, tofauti na dola milioni 36 zilizotajwa kwenye mkataba na kuamuliwa na mahakama. Badala ya Tanesco kulipa ‘capacity charge’ ya dola 50,000 kila siku umeme uzalishwe au la, udanganyifu wa mtaji ulipelekea Tanesco kuwa inalipa dola 100,000 kila siku tangu mwaka 2002,” alisema.
Zitto aliongeza kuwa kuanzia mwaka 2007 fedha hizo zilianza kuwekwa kwenye akaunti maalumu (escrow account) ya BoT.
Alisema kuwa mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete aliagiza kwamba ili kumaliza kabisa suala la mkataba wa kuuziana umeme wa IPTL, mitambo ya kampuni hiyo ichukuliwe na serikali. Mwaka 2006, 2007 na 2008 Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imekuwa ikitoa maagizo hayo hayo kuhusu suala la IPTL.
“Aprili 30 mwaka 2009, Kamati ya Bunge ya POAC ilipeleka mapendekezo bungeni kwamba IPTL ichukuliwe na serikali na fedha zilizopo katika escrow account zitumike pia kubadili mtambo ule kutoka mafuta mazito kwenda kutumia gesi asilia,” alisema.
Zitto aliongeza kuwa pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge na POAC ikatoa maelekezo maalumu kwa Gavana wa Benki Kuu kuwa fedha zilizopo escrow account zisitumike kwa namna yoyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa ili itumie gesi asilia.
Akifafanua chanzo cha escrow account, Zitto alisema baada ya mkataba wa IPTL kuingiwa, iligundulika kuwa kuna udanganyifu mkubwa ulifanyika katika kiwango cha mtaji wa kampuni hiyo, hivyo kufanya malipo wanayolipa Tanesco kwa IPTL kuwa makubwa mno.
Kwa mujibu wa Zitto katika kukokotoa gharama za uwekezaji (capacity charges) mtaji uliowekezwa katika IPTL ulisemwa ni dola milioni 36, ukweli ni kwamba IPTL waliweka dola 50 tu. Hivyo, capacity charge ya dola milioni 3 kwa mwezi haikupaswa kulipwa yote kwani kampuni iliendeshwa kwa mkopo kuliko mtaji wa wawekezaji.
Alisema kuwa mahakama ya kimataifa ya ICSID iliamua kuwa fedha zote za capacity charges ziwekwe Benki Kuu mpaka gharama halisi ziamuliwe na mahakama ndipo wahusika wagawane (Tanesco na IPTL).
“Akiba hiyo, nimeambiwa, ilifika dola milioni 250 kabla ya kuchukuliwa na kugawanywa kwa wanahisa na wanunuzi wa IPTL. Hivyo, kabla ya mgawo huu ilipaswa pesa ambazo Tanesco walikuwa wanalipa kama ziada ya capacity charges kwa IPTL zirejeshwe kwanza na zinazobakia ndio zilipwe kwa wadai na wanahisa.
“Kwa hali ilivyo sasa mnunuzi wa IPTL kapewa mitambo na fedha za kuinunua, ikiwemo fedha za Tanesco ambazo zilipaswa kurejeshwa,” alisema.
Zitto alihoji kama ziada ya fedha za malipo ya capacity charges zimerudi tanesco, mwekezaji mpya kapewa mkataba mpya wa kuuza umeme (PPA) kwa utaratibu gani wa zabuni, agizo la Rais na Bunge kwamba mitambo iwe ya umma limetupiliwa mbali kwa vigezo gani?
Aliitaka wizara husika itoe taarifa, CAG akague ili kuweka majibu kwa umma kupitia kamati ya PAC. Kwamba hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kuondoa wingu katika suala la IPTL ambalo toka limeanza miaka ya tisini limegubikwa na mazongezonge ya rushwa na uvundo wa kifisadi.

No comments:

Post a Comment