Rais Kikwete aagiza waliolipua Bomu Zanzibar wasakwe na kukamatwa haraka
RAIS Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki watu wote waliohusika katika ulipuaji bomu lililosababisha kifo na kujeruhi watu saba mjini Unguja, Zanzibar.
Rais
Kikwete ambaye amesema kitendo hicho ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote na
watu wote wapenda amani Bara na Visiwani, amekitaja kuwa ni cha woga
kisicho na ustaarabu, kisichokubalika katika dunia ya sasa.
Alisema hayo katika salamu za rambirambi alizotuma jana kwa Rais Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Bomu
hilo lilirushwa katika shughuli ya kidini iliyokuwa ikifanyika katika
eneo la Darajani , mjini Unguja. Miongoni mwa majeruhi, yumo mhubiri wa
amani ajulikanaye kama Sheikh Ahmed Haidari Jabir wa Zanzibar.
“Hicho
ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara
na Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na wala
hakikubaliki katika dunia ya sasa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hiki ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na ustaarabu wa aina yeyote ile.”
Alikemea
wanaofanya vitendo hivyo na akahimiza watu kuwa wastaarabu, wavumilivu
na kuheshimu imani na mitizamo ya watu wengine hata kama hawakubaliani
nao.
Akiendelea
kulaani, alisema amesikitishwa zaidi na watu hao wasio na ustaarabu
ambao wamefanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya kidini
ambapo ndipo mahali panapostahili amani, uvumilivu na unyenyekevu zaidi
kwa kuwa ni wakati ambapo binadamu anapofanya mawasiliano na muumba
wake.
Alihimiza
polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki wahusika wa
tukio hilo. Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya
Jinai wa Zanzibar, Yussfu Ilembo, aliyekufa papo hapo ni Muhammad
Mkombalaguha (26), mkazi wa Tanga.
Kutokana
na tukio hilo, polisi visiwani humo ilitangazia hali ya hatari kwa
watu waliohusika na shambulio hilo. Ilielezwa kwamba uchunguzi umeanzia
kwenye mabaki ya vitu vilivyokutwa katika eneo la tukio.
Miongoni
mwa vielelezo vilivyokusanywa ni pamoja na vipande vya mabaki ya gundi
ya karatasi na vitu vingine ambavyo vinasadikikwa vimetumika kutengeneza
bomu hilo.
Mtu
aliyekufa pamoja na majeruhi, walikutwa na mkasa huo wakati wakitoa
Msikiti wa Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha inayoswaliwa kuanzia
saa 1:45 usiku na kuendelea.
Baada
ya kumalizika ibada hiyo, walitoka msikitini na kufika eneo la Darajani
wakisubiri gari na ndipo mlipuko mkubwa uliposikika ambao unasadikiwa
kuwa ni bomu.
Katika
hatua nyingine, akiwa mkoani Dodoma juzi, Rais Kikwete aliwataka
Watanzania kuendelea kulinda na kupigania amani iliyopo kwa ustawi na
usalama wa nchi .
Rais
Kikwete alisema hayo juzi kwenye uzinduzi wa tamasha la uzalendo
lililoasisiwa na wasanii wa muziki na filamu nchini ikiwa ni pamoja na
uzinduzi wa video ya wimbo maalumu wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Alisema uzalendo kwa Watanzania ndiyo njia pekee ya kufanya taifa liendelee kutunukiwa hadhi ya kisiwa cha amani duniani.
Katika
tamasha hilo lililofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais Kikwete
alisema ili kuwaenzi waasisi wa taifa, ni lazima kudumisha misingi ya
amani na kujitolea kizalendo kulilinda na kulitetea taifa kama
walivyofanya waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amani Karume.
Pia aliwataka wasanii kutumia vizuri talanta walizojaliwa kufikisha ujumbe wenye uzalendo kwa Tanzania.

No comments:
Post a Comment