HAMZA KALALA: SERIKALI ITUPIE JICHO LA TATU MUZIKI
GWIJI wa muziki wa dansi nchini Hamza Kalala ‘Komandoo’ au ‘Mzee wa Madongo’, ambaye pia ni Kiongozi wa Bendi ya Bantu Group ya jijini Dar es Salaam, aliyetembelea chumba chetu cha habari Bamaga Mwenge hivi karibuni, amesema serikali inapaswa kutupia jicho la tatu au kuuangalia muziki wa dansi nchini kwa kuwa unatoa ajira kwa vijana.
Aidha, aliwataka vijana wa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva) kujifunza ala za muziki ili wawe wanamuziki kamili badala ya kutegemea kutengenezewa muziki kwenye kompyuta.
Baadhi ya mahojiano na waandishi yalikuwa kama ifuatavyo.
Mwandishi: Kabla ya yote tueleze historia yako kwa ufupi.
Kalala: Nilianza kupiga muziki mwaka 1966 na nimefanikiwa kuwa na wanamuziki wengi. Bendi ambazo nimepigia ni pamoja na Uda Jazz ‘Bayankata’, Vijana Jazz ‘Saga Rhumba’, Matimila Ochestra ‘Talakaka’, Washirika Band ‘Watunjatanjata’ na baadaye nikaanzisha Bendi ya Bantu Group.
Mwandishi: Ni sababu zipi zilikufanya uwe unahamahama?
Kalala: Hakuna sababu nyingine isipokuwa ni masilahi tu.
Mwandishi: Kuanzia mwaka 1966 mpaka leo ni miaka mingi upo katika fani ya muziki, umeweza kutunga nyimbo ngapi?
Kalala: Nimetunga nyimbo zaidi ya mia moja kama vile Ilikuwa Lifti Tu nikiwa Vijana Jazz, Tulizaliwa Wote, nikiwa Uda Jazz, Masido nikiwa Vijana Jazz na nyingine nyingi, kuzitaja zote tunaweza kujaza kurasa.
Mwandishi: Katika muziki wa dansi wewe unapiga solo gitaa, je, kuna ala nyingine unamudu kupiga?
Kalala: Licha ya solo gitaa, naweza kupiga besi gitaa, rithim gitaa, drums, saxophone, kinanda, tumba na kuimba ni trumpet tu ndiyo siwezi kuzipuliza.
Mwandishi: Katika muziki wa dansi ni wanamuziki gani wakipiga gitaa la solo ‘wanakukuna?’
Kalala: Ni wawili, Miraji Shakashia ambaye sasa yupo Twanga Pepeta na Yohana Wanted.
Mwandishi: Katika muziki wa kizazi kipya kuna mwanamuziki gani anakukosha.
Kalala: Ni Barnaba Elias, huyu namkubali kwa sababu anaimba vizuri na ana sauti nzuri lakini pia anapiga vizuri sana gitaa, nawaomba wanamuziki wengine wa muziki wa kizazi kipya wamuige kijana huyu. Ili kuthibitisha haya, mualikeni hapa mtathibitisha haya ninayoyasema.
Wanamuziki wa Bongo Fleva hivi sasa bendi yao ni kompyuta, kwa hiyo mtengeneza muziki akikataa kufanya hiyo kazi basi muimbaji yule anakuwa hana bendi, hili ni kosa kubwa wanalifanya. Miaka ijayo kama wataendelea kutojifunza ala, tutakuwa tunawategemea Wakongo kutupigia magitaa na ala nyingine na hii itakuwa mbaya sana.
Mwandishi: Hivi karibuni kulikuwa na Shindano la Kilimanjaro Music Awards, wewe kama mkongwe wa fani hiyo unalizungumziaje?
Kalala: Kwanza nitoe ushauri kwa waandaaji kwamba wanapaswa kufanya utafiti wa kuwapata washindi na wasitegemee kura.
Inapaswa mshindi anayeshinda tuzo awe anastahili kwa sababu kutegemea kupigiwa kura anaweza kupatikana mtu kutokana na ushabiki au mtu anaweza kuwa na watu wenye uwezo wakapiga kura nyingi sana kwa mtu asiyestahili. Nashauri pamoja na kura za watu utafiti ufanyike kwa kuwatembelea wanamuziki husika ili tuzo zitolewe kwa wanaostahili.
Mwandishi: Unashauri nini kuhusu wanamuziki wa zamani kuingizwa katika tuzo hizo?
Kalala: Lingekuwa jambo jema sana hata wanamuziki wa zamani wakatambuliwa kwa kushindanishwa na mshindi kupewa tuzo kwa sababu wana mchango mkubwa katika fani ya muziki.
Mwandishi: Unadhani kwa nini muziki wa dansi unafifia siku hizi?
Mwandishi: Katika siku za hivi karibuni bendi za muziki wa dansi zinafanya maonesho kwenye baa badala ya kwenye kumbi na mashabiki kulipa viingilio, huoni kuwa hilo linachangia kuua muziki huo?
Kalala: Hapana, muziki kwenye baa na kiingilio kuwa kinywaji unalipa, wala siyo tatizo. Mimi pia nafanya hivyo, kuna faida nzuri.
Mwandishi: Nakushukuru sana kwa kukubali wito wetu wa kufika katika ofisi zetu.
Kalala: Nawashukuru nanyi, nawaomba mnialike tena siku zijazo.
No comments:
Post a Comment